IDADI YA WANAFUNZI WATAKAOKOPESHWA YAONGEZEKA.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeongeza mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wengine 1,285 ambao awali walikosa mikopo hiyo.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa katika taarifa yake kwa umma jana, alisema kati ya wanafunzi hao, 789 ni wale ambao wamedahiliwa kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na 496 ni wanafunzi waliodahiliwa kupitia Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Awali waombaji 23,340 ndio waliopitishwa na Bodi hiyo kupata mikopo kwa mwaka huu wa masomo na kuwaacha waombaji 14,584 waliokosa mikopo hiyo kwa sababu mbalimbali zilizotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HLSB).

Uamuzi huo wa Serikali kuwapatia mikopo waombaji hao wa nyongeza, umefikiwa baada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kukutana na wawakilishi wa wanafunzi waliokosa mikopo.

Awali wanafunzi hao waliandamana hadi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambako waliwasilisha malalamiko yao ya kutoridhika na uamuzi wa Bodi hiyo kutowapatia mikopo hiyo.

Dk. Kawambwa katika taarifa hiyo alisema, baada ya wizara yake kukutana na wawakilishi wa wanafunzi waliokosa mikopo, waliielekeza Bodi hiyo kuchambua kwa kina orodha ya majina ya waombaji waliodahiliwa.
Waombaji hao ni wale ambao wamedahiliwa kupitia TCU ambao wametoka moja kwa moja kutoka shuleni na waombaji waliodahiliwa kupitia NACTE ambao hawakuingizwa kwenye mchakato wa kupatiwa mikopo hapo awali.

“Hivyo uchambuzi huo umewezesha kupatikana ongezeko la wanafunzi 1,285 kutengewa mikopo,” ilisema taarifa hiyo na kufafanua kuwa orodha ya majina hayo itawekwa kwenye tovuti ya Bodi hiyo.

Dk. Kawambwa katika taarifa hiyo alifafanua kuwa wanafunzi 1,115 waliodahiliwa katika fani ya ualimu wa sayansi, ualimu wa hesabu na sayansi za tiba ambao hawajapata mikopo kutokana na kasoro kadhaa kwenye fomu zao, wamepewa wiki mbili kurekebisha kasoro hizo.

Alitaja kasoro hizo kuwa ni kutosainiwa fomu za maombi au kutoambatanisha vyeti vya kuzaliwa na kuongeza kuwa wakikamilisha taratibu hizo katika kipindi hicho, watakuwa wamekidhi vigezo vya kutengewa mikopo.

Wakati huo huo, Dk. Kawambwa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa makini utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuhakikisha lengo la mikopo kwa wanafunzi linafanikiwa.

Dk.Kawambwa alisema hayo wakati alipokutana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ramadhan Abdalla Shaaban ofisini kwake Mazizini mjini Unguja.

Baadhi ya sababu za kunyimwa mikopo ni waombaji zaidi ya mmoja kutumia nambari za mitihani wa kidato cha nne zinazofanana au zilizokosewa na waombaji wengine kushindwa kuambatanisha cheti cha kuzaliwa kuthibitisha uraia wa muombaji. “Huwezi kumpa mkopo mwanafunzi ambaye hana cheti cha kuzaliwa,” alisema.

Habari zaidi Tembelea http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21959&cat=kitaifa

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s