WANAFUNZI UDSM WAZOMEA UJIO WA JK JANA KATIKA MAADHIMISHO YA CHUO HICHO.

Fidelis Butahe, Mwananchi.
WANAFUNZI wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) jana walichafua hali ya hewa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho baada ya kumzomea Rais Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete ambaye alikuwa ameambatana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa pamoja na viongozi wengine wa Serikali alikutwa na zomeazomea  hiyo saa 6:23 mchana wakati akiingia katika Ukumbi wa Nkrumah ambapo yalifanyika maadhimisho hayo.  Wanafunzi hao mbali na kumzomea Rais huyo wa awamu ya nne pia walikuwa wamebeba  mabango yenye ujumbe mbalimbali huku wakiimba, “Kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi, hatukutaki ondoka,”.

Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa, ‘’Wao walisoma bure sisi tunalala nje, Miaka 50 ya uhuru mikopo hatupati, Tusiilipe Dowans, Wanafundisha UDSM makazi Bagamoyo je ni haki?, Kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi.

Awali wanafunzi hao walionekana wakiwa wameshika mabango hayo lakini walizuiwa na polisi na kuelezwa kuwa kama ni ujumbe tayari ulishafika hivyo waendelee na shughuli nyingine.

  Hata hivyo, wanafunzi hao ambao hawakutaka kutaja majina yao walizunguka nyuma ya Ukumbi wa Nkrumah na kuyaficha mabango hayo, huku wengine wakijipanga tayari kwa kumpokea Rais Kikwete ambaye alikuwa bado hajafika eneo hilo.

Mara baada ya Rais Kikwete kufika chuoni hapo alikwenda kusaini katika kitabu cha wageni na wakati akielekea katika ukumbi huo huku akipunga mkono, wanafunzi hao walikuwa kimya.

Rais Kikwete wakati akiendelea kuwapungia mkono wanafunzi hao, walianza kumzomea na kutoa mabango yao waliyokuwa wameyaficha huku wakiimba, “Kama sio juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi”.

Polisi waliokuwa eneo hilo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana  walilazimika kutumia busara kuwanyamazisha wanafunzi hao ambao waliendelea kuzomea na kuimba licha ya kuwa Rais Kikwete alikuwa ameshaingia katika ukumbi huo.

 Wakati shughuli za maadhimisho hayo zikiwa zinaendelea wanafunzi hao walikuwa bado wakiimba nyimbo hizo na kuzomea, mpaka walipoombwa kutoendelea kuimba na baadhi ya polisi ambao waliwaeleza kuwa kuzomea hakuwezi kuwaletea mikopo vyuoni, bali wajenge hoja za msingi na kuziwasilisha sehemu husika.

Hata wakati Rais Kikwete akisoma hotuba yake na kugusia maendeleo ya chuo hicho pamoja na uboreshwaji wa utoaji mikopo vyuoni, wanafunzi hao waliokuwa wakifuatilia hotuba hiyo kupitia Televisheni kubwa walikuwa wakizomea.

“Hivi Rais anajua jinsi tunavyopigika hapa chuoni, wengine inaonekana tumepewa mikopo, lakini mpaka leo hatujapata, hivi anajua tunaishi vipi huyu, anajua tunalala wapi,” walisikika wakisema baadhi ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alisema kuwa kilichofanywa na wanafunzi hao kinatakiwa kutazamwa kwa macho mawili.

Mnyika alisema kuwa ahadi zilizotolewa na Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya chuo hicho zinatakiwa kutekelezwa na kufafanua kuwa hata katika utawala wa Mwalimu Nyerere matatizo vyuoni yalikuwapo na kwamba dawa ni kuyatatua.

  Akizungumzia kitendo cha wanafunzi hao kumzomea Rais Kikwete mbele ya Rais Museveni, Mnyika alisema kuwa hilo ni jambo la kawaida kwa kuwa Museveni amewahi kusoma katika chuo hicho na anajua harakati za wanafunzi.
“Wakati Museveni akisoma alikuwa na kikundi chake ambacho kilikuwa na msimamo mkali na kutoa kauli za kimapinduzi kwa viongozi mbalimbali wa Afrika, Museveni anakijua hiki chuo,”

Rais Kikwete akiwasili ukumbini, MAADHIMISHO ya mika 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yamezinduliwa rasmi leo na Rais Dkt. Jakaya Kikwete akiwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika Ukumbi wa Nkrumah uliyopo chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala (kulia) akiwa na Rais Dkt Jakaya Kikwete (wa tatu kushoto) pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wakati wa maadhimisho hayo.

Baadhi ya wanafunzi wa UDSM wakifuatilia Maadhimisho hayo chuoni hapo.

 

Ujumbe huo jamani kutoka kwa wanaUDSM

Watoa maamuzi mmeusoma?

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s