MAHAFALI CHUO KUKUU KISHIRIKI CHA ELIMU MKWAWA: Serikali kuajiri walimu 23,000

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo amesema Serikali itaajiri walimu wapya 23,000 katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha. Alirudia ahadi ya Serikali ya kutoa kile alichokiita kitita cha Sh 500,000 kwa kila mwalimu atakayepata ajira mpya katika maeneo yenye mazingira magumu. Aliyasema hayo juzi kwenye Mahafali ya Tatu ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa kilichopo mjini Iringa mkoani Iringa.

Katika mahafali hayo, wanafunzi 420 kati ya 654 waliojiunga na chuo hicho miaka mitatu iliyopita, wamehitimu na kutunukiwa shahada za ualimu katika fani nne; Shahada ya Elimu ya Jamii na Ualimu, Shahada ya Elimu ya Sayansi za Jamii, Shahada ya Sayansi na Ualimu na Shahada ya Elimu katika Sayansi.

“Najua nanyi mnaotunukiwa shahada zenu hii leo, mtakuwa katika kundi hilo la walimu watakaopata ajira mpya, rai yangu kwenu zingatieni maadili, jitofautisheni na wale wanaolegeza suruali na kuvaa vinguo vifupi,” Mulugo alisema na kuwataka walimu hao kuyakubali mazingira ya kazi watakakopangiwa.

Akiwapongeza wahitimu hao, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Philemon Mushi aliishukuru Serikali kwa ushirikiano wake mzuri, lakini alisema kinakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ufinyu wa ruzuku kutoka serikalini. “Kwa mfano kwa mwaka wa fedha uliopita, Serikali ilikipa chuo chetu jumla ya shilingi bilioni 1.5 sawa na asilimia 36.5 ya shilingi bilioni 4.5 zilizoidhinishwa na Serikali, upungufu huu umesababisha kukwama kwa baadhi ya miradi ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu na hivyo kuathiri shughuli za kitaaluma,” alisema.

Alisema chuo hicho kinakabiliwa pia na uhaba mkubwa wa wahadhiri hivyo kulazimika kutumia wahadhiri wa muda ambao ni gharama kwani chuo hulazimika kutumia karibu nusu ya bajeti yake ya matumizi mengineyo ambayo nayo imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kuwalipa wahadhiri hao.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho Mkwawa ni chuo chake kishiriki, Peter Ngumbulu alisema pamoja na kutambua changamoto nyingi zinazoikabili Serikali katika kupata fedha za kutosheleza mahitaji mengi muhimu, bado wanaiomba iendelee kuunga mkono shughuli zinazoendelea na zile zitakazoanzishwa chuoni hapo. “Hiyo ni pamoja na ukarabati na upanuzi wa madarasa, nyumba za wafanyakazi na mabweni ya wanafunzi ili kukiwezesha chuo kutekeleza majukumu yake ipasavyo,” alisema. Mwaka 2005/06, chuo hicho kilipokuwa kinaanzishwa kilikuwa na wanafunzi 917 na hadi mwaka huu kina jumla ya wanafunzi 2,345 wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s