KUTOKA SAUT: KONGAMANO LA MIAKA 50 YA UHURU LAFANYIKA HII LEO, MADA IKIWA NI UHURU, KATIBA NA HAKI ZA BINAADAMU KATIKA MIAKA 50 YA UHURU, MAFANIKIO NA CHANGAMOTO.

Chuo cha Mtakatifu Agustino kwa kushirikiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora leo wamefanya kongamano kubwa la kujadili Miaka 50 ya uhuru lililolenga juu ya “uhuru, katiba na haki za binaadamu katika miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara mafanikio na changamoto” kongamano lililofanyika katika ukumbi wa M13 chuoni hapo.

Akiwa mzungumzaji wa kwanza katika kutoa tafakari juu ya uhuru: Nini maana ya uhuru? Mgeni rasmi wa kongamano hilo Padri Dk. Charles Kitima alieleza maana na historia nzima ya kupigania uhuru aliyofanywa na waasisi wa nchi hii chini ya uongozi shupavu wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kugusia Azimio la Busara lililofikiwa Tabora miaka ya 1958 mkoani Tabora.

“Uhuru wa Tanzania ulipatikana kwa watu kuamua na kutenda harakati za kupigania uhuru bila ya kumwaga damu bila ya viongozi kudanganya wananchi na bila ya kuleta usanii kwa wananchi, Nyerere hakuwa na masilahi binafsi katika maamuzi ya kitaifa, hakuwa na maamuzi binafsi juu ya maamuzi ya Azimio la Busara mkoani Tabora 1958 ndio maana alileta uhuru bila kumwaga damu ya mtu” Alisema.

“Vijana uhuru wa Kisiasa na kijamii unateteleka kwa sababu hakuna uhuru wa Kiuchumi na kama vijana hamtatetea uhuru wa kiuchumi wa nchi hii basi vizazi vinavyokuja vitaishi kwenye matatizo makubwa, Nyerere aliacha migodi isichimbwe ili kusubiria wazawa wa nchi hii kuja kuichimba, ni lazima kupigania uhuru wa kiuchumi nchi hii ili kumiliki vitega uchumi vyetu wenyewe vya nchi yetu”. Alisema.

Dk. Kitima alisema pia nchi imekubali vyama vingi ni lazima serikali zibadilishane madaraka , watu wasidanganyike kwamba chama kimoja tu ndio kinaweza kuendelea kutawala. Akatoa mfano wa Mwl. Nyerere kwamba Nyerere aliona umuhimu wa kubadilishana madaraka ndio maana aliweza kuachia madaraka kwa hiyari ili kupisha watu wengine waweze kuendelea kuongoza nchi hii hivyo wananchi wasiwe na uwoga wa kubadilisha uongozi kwa ksingizio amani haitakuwepo kwani huo ni ufinyu wa kimawazo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt. Agustino Padri Dk. Charles Kitima akitoa tafakari katika kongamano hilo. "Vijana wanatoa mawazo mazuri juu ya kuendeleza nchi yetu kwenye makongamano kama haya, lakini wanashindwa kutoa elimu kwa watu wote wa tabaka la chini hasa vijijini juu ya jinsi gani wanaweza kufanya mabadaliko nchini, na vijana hampigi kura za kuchagua viongozi wa nchii hii kazi yenu ni kuchangia maoni tu katika mijadala ya kitaifa" Alisema.

Mhadhiri Daudi Mwita Nyamaka kutoka kitivo cha Sheria SAUT, akitoa mada juu ya historia ya Katiba Tanzania "Katiba ya 1977 ndio katiba iliyofanyiwa marekebisho mara 14 ambapo ni marekebisho mengi kuliko katiba nyengine zilizopita lakini bado ina changamoto nyingi, umiliki wa katiba haupo kwa wananchi, haitoi fursa ya wananchi kumiliki Taifa lao, Kero za muungano hazijatatuliwa, haitoi ushiriki wa wananchi katika uongozi waliouchagua na haitoi ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya dola na wananchi. Hatuna budi ya kutengeneza katiba ya wananchi, Watanzania amkeni ili kuishinikiza serikali kuleta katiba ya wananchi"

Mhadhiri msaidizi wa SAUT, Innocent Ndaga akizungumzia Mafanikio na Changamoto kuhusu historia ya Haki za Binaadamu katika katiba ya Tanzania.

Mhadhiri msaidizi kutoka kitivo cha sheria SAUT, Raphael Kamuli, akizungumzia historia ya haki za binadamu katika katiba ya Tanzania. Akimnukuu mpiganaji wa Haki za Binaadamu katika hitimisho la Mada yake alisema "Giza haliwezi kuondoa giza bali mwanga ndio unaweza kuondoa giza" watanzania tuwe mwanga wa kuondoa giza lililopo nchini, pia aliendelea kunukuu "siku za maisha ya binadamu huisha pale binadamu ataanza kukalia kimya mambo ya msingi" Watanzania tusikae kimya tupaze sauti zetu kwani sauti za wengi ni sauti za Mungu.

Peter John Bega mwanafunzi wa Mwaka wa kwanza shahada ya sheria akitoa maoni yake. Alisema "Tume ya haki za binadamu nayo ichaguliwe na wananchi ili mwisho wa siku nayo iwajibike kwa wananchi"

Bi. Matulile Wabulala mwanafunzi wa shahada ya sheria mwaka wa tatu SAUT akichangia mada juu ya katiba mpya, alisema "Tatizo ni elimu, katika katiba mpya ningependa itoe msisitizo juu ya elimu za viongozi wa nchi hii kwani viwango vya elimu ni vidogo ndio maana wanasaini mikataba mibovu hivyo katika katiba ni lazima iseme kiwango cha elimu cha viongozi wetu".

Wanajamii ya SAUT wakifuatilia mdahalo huo.

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s