CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM CHAFUKUZA WANAFUNZI 43.

Askari wakikabiliana na mwanafunzi huyu wa kike kwenye yaliyotoke mwezi 11, 2011, Maandamano yaliyopelekea wanafunzi 43 wa UDSM kufukuzwa Chuo.

CHUO  Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimewafukuza wanafunzi 43 na kuendelea kufuatilia nyendo za wengine tisa, baada ya kubainika kuwa walihusika katika matukio mbalimbali ya vurugu na uhalifu chuoni hapo. Kati ya wanafunzi hao, wanane walikuwa  wamesimashiwa masomo kwa muda wa miezi tisa na 35 walisimamishwa ili kusubiri kumalizika kwa kesi zao zilizopo mahakamani.

Uamuzi huo umekuja ikiwa zimepita siku mbili tangu baadhi ya wanafunzi chuoni hapo, kuvamia  jengo la Ofisi  za utawala la chuo hicho na kuwazuia maofisa na wafanyakazi wa chuo kutoka au kuingia ndani, hadi watakapoletewa taarifa za pesa zao kutoka Bodi ya Mikopo(TCU).

Wanafunzi hao waliokuwa wanaendeleza mgomo wao ulioanza Jumatatu wiki hii wakidai taarifa za kwa nini pesa zao zinachelewa wakati bodi ya mikopo, ilishasema wamezileta chuoni hapo. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema hatua hiyo imekuja baada ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani chuoni hapo tangu  mwanzo wa juma hili. 

“Desemba 13 (Jumanne) Kamati ya Wakuu wa Chuo na Shule Kuu zilizoko kampasi kuu ya Mlimani walifanya kikao cha dharura na kufanya mapendekezo kuhusu hatua za kuchukuliwa ili kusitisha uhalifu chuoni,”alisema Mukandala na kuongeza:

“Siku hiyo hiyo Baraza la Chuo nalo lilifanya kikao cha dharura na kutathimi mwelekeo wa chuo na kupitia mapendekezo yaliyoletwa na Kamati ya Wakuu wa chuo na shule kuu na kutoa maamuzi.”. Profesa Mukandala alisema, maamuzi yaliyotolewa na vikao hivyo ni pamoja na kuwafukuza wanafunzi hao 43 na kuchukua hatua za kuongeza ulinzi kwa muda katika maeneo muhimu ya chuo ili wanafunzi walio wengi waendelee kusoma bila kusumbuliwa.

Alisema kati ya wanafunzi hao 43, wanafunzi wanane ni wale ambao walisimamishwa masomo kwa muda wa miezi tisa, lakini waliendelea kuonekana maeneo mbalimbali ya chuo hicho huku wakilazimisha kuonana na uongozi. “Kuna hawa 35 ambao ni kati ya wale wanafunzi 51 waliokuwa na kesi mahakamani nao wamefukuzwa, kati ya hao 51 ilibainika kwamba watatu  hawakuwa wanafunzi wa UDSM, hivyo wanafunzi walikuwa 48 tu,” alisema Profesa Mukandala.

Alisema kuwa kuna wanafunzi tisa ambao mpaka sasa uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili, unaendelea na kufafanua kuwa kati yao, wanne wanatuhumiwa kuwa vinara wa kuongoza vurugu zilizotokea Jumatatu na Jumanne wiki hii na watano ni wale wanaokabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani.

  “Kati ya hao wanafunzi wanne ambao wako katika uchunguzi, mmoja alivunja vioo vya mabasi ya kubebea wanafunzi na mwingine alimchapa fimbo tumboni mwanafunzi mjamzito na kumsababishia maumivu makali.

Pia yupo aliyemmwagia profesa maji akiwa darasani. Yeye ni miongoni mwa wale 43 waliotimuliwa,” alisema Profesa Mukandala. Vurugu Akizungumzia vurugu, uharibifu na uvunjifu wa amani uliofanywa na wanafunzi hao, Profesa Mukandala alisema walikimwagia chakula vumbi, kuwapiga wafanyakazi wa mgahawa, kuharibu majokofu na kushambulia mabasi yaliyopita eneo la chuo yakiwemo yanayobeba wanafunzi, hali iliyosababisha huduma hizo kukosekana kwa siku mbili.

“Wanaotoa huduma ya mabasi kutoka Hosteli ya Mabibo waligoma kutoa huduma hiyo, hata wanaoendesha mgahawa nao waligoma kutoa huduma ya chakula jambo ambalo lilileta usumbufu kwa wanafunzi, ila kwa sasa hali ni shwari,” alisema Profesa Mukandala.

Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, matukio hayo ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza kutokea mwanzoni mwa Septemba mwaka huu na kwamba vurugu hizo zilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi ambao walipata wafuasi wachache na kuvuruga shughuli za chuo hicho.     

Madai ya Wanafunzi Profesa Mukandala alisema awali madai ya wanafunzi hao yalikuwa ni kuondolewa adhabu za kinidhamu walizopewa wenzao wachache kwa mujibu wa kanuni na sheria za chuo,  lakini baadaye wakageukia suala la kupatiwa fedha zao za malazi na chakula kwa kipindi cha kuanzia Desemba 10 mwaka huu. Alifafanua kuwa fedha hizo hutolewa kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza ilikuwa Sh 4.2 bilioni ambayo ilitolewa kwa wanafunzi wa Kampasi ya Mlimani na kwamba ziliingizwa katika akaunti tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Awamu ya pili ilikuwa ni Sh 700Milioni kwa wanafunzi wa Uhandisi, fedha hizo ziliingizwa jana (juzi) katika akaunti za wanafunzi na awamu ya tatu ilikuwa Sh 200Milioni kwa wanafunzi wanaosoma Uandishi wa Habari ambazo ziliingizwa katika akaunti Desemba 12,” alisema Profesa Mukandala.

Alisema katika kipindi hicho chote, Baraza la Chuo lilikutana kujadili hali hiyo na kuwataka wanafunzi hao kutoendelea na mgomo na kuvunja taratibu za chuo na kuwaonya kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, lakini baadhi yao hawakuonyesha kujali.  

Onyo kali Profesa Mukandala alitumia fursa hiyo kuonya kuwa mwanafunzi yoyote atakayefanya tendo la kihalifu ikiwa ni pamoja na kujaribu kuwatisha wenzake au kuendesha mkutano nje ya taratibu za chuo, atafukuzwa.  “Pia yanafanyika mawasiliano na Bodi ya Mikopo (TCU) ili wanafunzi waliofukuzwa chuo kutokana na uhalifu wasipate tena mkopo wa Serikali wala kuruhusiwa kusoma katika chuo chochote cha umma,” alisema Mukandala.

Polisi waweka kambi Wakati huohuo, polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wameweka kambi katika eneo la Chuo Kikuu cha Ardhi kilichoko jirani na Chuo Kikuu hicho cha Dar es Salaam, ili kukabiliana na vurugu za wanafunzi. kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi lilishuhudia magari manne ya FFU yakiwa yameegeshwa eneo hilo sambamba na gari linalobeba maji ya kuwasha.

NA: Fidelis Butahe, Gazeti la Mwananchi.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s