BAADA YA UDSM: CHUO KIKUU MUHIMBILI NACHO CHASIMAMISHA WANAFUNZI 66.


SIKU moja baada ya Chuo Kikuu cha Dares Salaam kuwafukuza wanafunzi 43 , Uongozi wa  Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), umewasimamisha masomo wanafunzi 66 kwa tuhuma za kuwa vinara wa vurugu chuoni hapo. Mbali na hatua hiyo, uongozi wa chuo hicho umeeleza kuwa mipango ya vitisho na uvunjifu wa amani chuoni hapo, bado ipo na inaleta hofu kwa walimu na wanafunzi wengine wanaoendelea na masomo.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo, alisema jana kuwa wanafunzi waliosimamishwa ni wale waliohusika katika vurugu zilizotokea chuoni hapo Desemba 8, mwaka huu wakati wa sherehe ya utafiti na Desemba 10 wakati wa mahafali na Jumatatu wiki hii.

Profesa Pallangyo alisema wanafunzi hao wamesimamishwa masomo kwa muda usiojulikana hadi hapo uchunguzi utakapokamilika na kwamba matokeo ya uchunguzi huo ndio yatakayoamua kama wanafunzi hao waendelee na masomo au la, alisema. “Tunao ushahidi kwamba wamefanya makosa, lakini na wao watapewa nafasi ya kuja kujitetea na inawezekana idadi hiyo ikaongezeka na tutatumia taratibu za ndani za kinidhamu,” alifafanua Profesa Pallangyo.

Alisema kati ya wanafunzi hao ambao ni wa mwaka wa tatu na wa tano kuna msichana mmoja tu  mmoja aliyekumbwa na adhabu hiyo.Aliongeza kwamba, uongozi wa chuo hicho una ushahidi wa mkanda wa video na taarifa zingine kutoka vyombo vya usalama. Alieleza kuwa chanzo cha vurugu hizo ni madai ya wanafunzi hao kutaka kurejeshewa serikali yao wanafunzi (MUHASSO) iliyovunjwa na Baraza la chuo hicho.

Profesa Pallangyo alisema shughuli za serikali hiyo zilisitishwa tangu Juni mwaka huu na baraza la chuo hicho kutokana na kukaidi maagizo ya Serikali yaliyotaka vyuo vikuu vyote kubadili katiba zao. Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo, mwaka 2009 serikali ilitoa waraka kwa serikali za wanafunzi katika vyuo vikuu vyote kwamba wabadilishe katiba zao, lakini serikali nyingi za wanafunzi ikiwemo Muhasso, hawakukubaliana na uamuzi huo.

“Tuliongea nao kwenye baraza la chuo na kuwashawishi wabadili katiba yao ili iendane na waraka wa serikali, lakini walikataa na Februari mwaka huu Waziri wa Elimu alikuja hapa na kuzungumza nao lakini walikataa,” alisema. Makamu Mkuu huyo alisema vyuo vingine kama Dodoma, Mzumbe na Mkwawa walikubali kubadilisha katiba zao lakini Muhasso waliendelea na msimamo wao wa kukataa.

Alisema baada ya baraza la chuo kusitisha shughuli za Muhasso, Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi, Gervas Shayo alikwenda mahakamani kufungua kesi akiwashtaki Makamu Mkuu wa chuo hicho, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambayo humu yake haijatolewa, alisema. Alisema uongozi wa chuo uliwataka wanafunzi hao waiondoe kesi mahakamani ili wakae na kujadiliana namna ya kurejesha Muhasso, lakini bado walikataa na kwamba, waliharibu sherehe za utafiti pamoja na mahafali.

Alisema pia vurugu hizo zinaweza kuwa na athari kubwa hasa kwa wafadhili wao wakubwa ambao ni serikali ya Sweden, ambao walikuwepo Desemba 8, wakati wa sherehe ya utafiti chuoni hapo. Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eligius Lyamuya alisema mipango ya kutishia amani bado ipo chuoni hapo na kwamba, inaleta hofu kwa walimu na kwa wanafunzi ambao wako tayari kuendelea na masomo.

UDSM hali bado tete Wakati hayo yakiendelea MUHAS, Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (DARUSO), imesema haijaridhishwa na hatua ya kufukuzwa wenzao 43 hivyo inajipanga kuwatetea wenzao hao kwa nguvu zote.

Juzi uongozi wa UDSM ulitangaza kuwafukuza wanafunzi 43 na kuendelea kufuatilia nyendo za wengine tisa, baada ya kubainika kuwa walihusika katika matukio mbalimbali ya vurugu na uhalifu chuoni hapo. Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani chuoni hapo tangu  mwanzo wa juma hili.

Adhabu waliyopewa wenzetu ni kubwa kuliko makosa wanayotuhumiwa kuyafanya. Hatuikubali, tunaipinga na tutachukua hatua kuhakikisha kwamba wanarudi chuoni kuendelea na masomo yao,” Rais wa Daruso. Simon Kilawa alisema jana. Alieleza kuwa hatua ya kwanza watakayoichukua ni kuzungumza na uongozi wa chuo kuhusu adhabu hiyo na kuongeza; “Katika hili, tayari tumeshakubaliwa kwa sharti kwamba katika mazungumzo hayo kusiibuke vurugu yoyote.”

Alisema kama mazungumzo yao na uongozi hayatafikia mwafaka, watalipeleka suala hilo katika Bunge la wanafunzi ambalo ndio lenye maamuzi ya mwisho.“Kwa sasa siwezi kusema nini kitakachoamuliwa na Bunge hili na mpaka sasa, hatuwezi kuchukua hatua zozote kwa kuwa bado hatujazungumza na uongozi (utawala) na kujua nini hatma ya wenzetu,” alisema Kilawa. Kwa mujibu wa Kilawa, Daruso iliuomba uongozi wa chuo kuwaruhusu wanafunzi 35 waliosimamishwa masomo kutokana na kuwa na kesi mahakamani waendelee na masomo, lakini wameshangaa hatua zilizochukuliwa za kuwafukuza wakati walikubaliwa kuendelea na masomo.

Jumatatu wiki hii wanafunzi hao walifanya mgomo wakidai taarifa za kwa nini pesa zao zinachelewa wakati Bodi ya Mikopo (HESLB), ilishasema wamezileta chuoni. Kutokana na hali hiyo, wanafunzi hao walivamia jengo la Ofisi za Utawala na kuwazuia maofisa na wafanyakazi wa chuo hicho kutoka au kuingia ndani, hadi watakapoletewa taarifa za pesa zao kutoka TCU.

Uongozi
Akizungumzia vurugu, uharibifu na uvunjifu wa amani uliofanywa na wanafunzi hao juzi, Profesa Mukandala alisema walimwagia vumbi chakula, kuwapiga wafanyakazi wa mgahawa, kuharibu majokofu na kushambulia mabasi yaliyopita eneo la chuo yakiwemo yanayobeba wanafunzi, hali iliyosababisha huduma hizo kukosekana kwa siku mbili.

Kwa mujibu wa Profesa Mukandala, matukio hayo ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza kutokea mwanzoni mwa Septemba mwaka huu na kwamba vurugu hizo zilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi ambao walipata wafuasi wachache na kuvuruga shughuli za chuo hicho.

Fidelis Butahe
Nora Damian

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s