UDSM YAWAGEUKA WANAFUNZI 41; YAJITOA KUWADHAMINI.

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umejivua udhamini wa wanafunzi 41 kati ya 51 wanaokabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ya maandamano na kufanya mkusanyiko haramu.

Akiwasilisha barua hiyo jana kutoka kwa uongozi huo, mwakilishi wake, Ambinyiel Maro alidai mbele ya Hakimu Stewart Sanga kuwa amepewa barua hiyo na uongozi wa chuo
kuomba kujivua udhamini.

Mahakama hiyo ilipokea maombi hayo, lakini Hakimu Sanga alisema anatoa nafasi mpaka Januari 10, mwakani kwa wanafunzi hao 41 kutafuta wadhamini wengine kuliko kuwarudisha rumande.

“Kisheria haitakuwa haki kupokonya udhamini kwa washitakiwa hao kwasababu imekuwa ni ghafla leo hawakujiandaa , hawakujua kama kuna barua hiyo,” alisema Hakimu huyo.

Alisema anatoa tahadhari tarehe hiyo wajiandae kuja na wadhamini kwa masharti yale yaliyowekwa awali na ambaye hatakuwa na mdhamini atakuwa amevunja masharti ya
dhamana, hivyo ataenda rumande.

Masharti yaliyowekwa ni kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika sambamba na kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni moja kwa kila mshitakiwa.

Hata hivyo, wanafunzi hao walionekana kuwa na maswali mengi na kunyoosha mikono yao kutaka kuuliza, lakini Hakimu Sanga alisema yeye sio msikilizaji wa kesi hiyo, hivyo hawezi kuwa na majibu wasubiri siku ambayo atakuwepo Hakimu mhusika wa kesi, Waliarwande Lema.

Kesi hiyo imepangwa kusomwa maelezo ya awali Januari 10, mwakani. Wanafunzi 50 wako nje kwa dhamana isipokuwa Said John ambaye yuko mahabusu.

Novemba 14, mwaka huu, wanafunzi hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kudaiwa kuwa katika eneo la Mlimani, kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Shitaka jingine walidaiwa kukaidi amri ya askari walipoambiwa watawanyike. Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala wiki iliyopita alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 51 waliokuwa wamefikishwa Kisutu, 43 kati yao ndio waliofukuzwa, watatu sio wanafunzi wa chuo
hicho, tisa hawajasikilizwa na Baraza la Chuo hicho na kutolewa mapendekezo.

Alisema matukio yaliyojiri ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani ambapo kila mara vitendo hivyo vilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi na hatimaye kupata wafuasi katika kuvuruga shughuli za chuo.

Alisema madai ya wanafunzi waliokuwa wakiendesha vurugu hizo, yamekuwa yakibadilika kila kukicha ambapo mwanzo walidai mikopo ya wanafunzi waliochaguliwa katika mwaka huu wa masomo na ambao hawakupata mikopo, baadaye dai kubwa likawa ni kuachiwa huru wenzao waliokamatwa na kufunguliwa mashitaka kutokana na kuendesha maandamano kinyume cha sheria na kukaidi amri ya Polisi ya kutawanyika.

Profesa Mukandala alisema katika siku mbili za vurugu madai ya awali yalikuwa kuondolewa kwa adhabu za kinidhamu walizopewa wenzao wachache kwa mujibu wa Kanuni na Sheria za Chuo, lakini baadaye wakageukia suala la kupatiwa fedha za malazi na chakula kuanzia Desemba 10, mwaka huu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s